Uhalifu wa mtandaoni unaoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, serikali imeweka mkakati kuutokomeza.
Mkakati huo unahusisha timu ya pamoja inayoundwa na taasisi za serikali, ikiwamo Wizara ya Habari, Jeshi la Polisi na mahakama kuwashughulikia wahalifu kwa mbinu za kidigiti.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amebainisha hayo bungeni jijini hapa jana, alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.
Bunge limeidhinisha makadirio hayo, Sh. bilioni 180.92 zikitengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi tisa inayolenga kuimarisha utoaji huduma za uhakika na za gharama nafuu za habari, kuweka mazingira yanayokuza ubunifu katika kubadilisha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijiti.
Waziri Nape amesema fedha hizo zitatumika kutekeleza mipango mbalimbali ikiwamo kujenga maabara za akili mnemba (AI) na matumizi ya roboti nchini.
Amesema kwa mwaka ujao wa fedha, pia wamepanga kujenga mfumo wa kufungamanisha taarifa za kila mwananchi ili kuwa na akaunti ya kidijiti itakayomwezesha kutumia huduma mbalimbali za kidijiti nchini.