Serikali inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu namna bora ya uanzishwaji wa Skimu ya Bima za Kilimo nchini kwa kuangalia utaratibu wa sheria, uendeshaji na gharama za utoaji wa bima za aina hiyo.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ulyankulu Mhe. Rehema Juma Migilla, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuanzisha bima ya kilimo kwa wakulima nchini.
Mhe. Chande alisema kuwa Serikali itaanzisha Skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo kwa kuzingatia matokeo ya upembuzi yakinifu unaoendelea katika maeneo yaliyobainishwa ili kuwa na ufanisi katika utekelezaji wake.
“Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali pia imeendelea kuratibu juhudi za uanzishwaji wa Skimu ya Taifa ya Bima za Kilimo kwa kuanzishwa kwa Konsotia ya Kampuni za Bima ya Kilimo nchini”, alieleza Mhe. Chande.
Alisema kuwa Konsotia ya Kampuni za Bima ya Kilimo nchini itahusika na utoaji wa pamoja wa bima zote za kilimo nchini ikiwemo bima zitakazosimamiwa na skimu ya bima za kilimo ambayo tayari ilizinduliwa rasmi tarehe 1 Julai 2023.