Serikali imesema inachukua hatua mbalimbali za kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo wilayani Kilosa mkoani Morogoro ikiwemo kupanda miti kuzunguka bwawa hilo katika eneo la hifadhi ndani ya eneo la mita 60.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 06 Juni, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mikumi Mhe. Dennis Londo aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo ili liweze kutumika kwa shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo.
Mhe. Khamis akiendelea kujibu swali hilo amesema katika kipindi cha msimu wa mvua wa 2024/25, halmashauri kwa kushirikiana na Bonde la Wami- Ruvu imepanga kupanda miti 5,000 ili kuongeza uoto wa asili na kuzuia mmomonyoko wa udongo katika maeneo yanayozunguka bwawa.
Ametaja mipango mingine kuwa ni kulinda eneo la hifadhi ya bwawa ndani ya mita 60 kuzunguka bwawa dhidi ya shughuli zisizoendelevu kwa kuendesha doria za mara kwa mara na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi katika vijiji vinavyonufaika na bwawa husika hususan kilimo na ufugaji endelevu.
Naibu Waziri Khamis ameongeza kuwa katika kuhakikisha wananchi wananufaika na bwawa hilo hususan shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeunda kikundi cha watunzaji wa mazingira na rasilimali za bwawa.
“Moja ya jukumu la kikundi hiki ni kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji na rasilimali za uvuvi katika bwawa,” amesema Naibu Waziri huku akifafanua kuwa katika kuboresha maeneo ya mwalo wa eneo hilo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25, Hamlashauri imetenga bajeti ya shilingi milioni 4 ili kukarabati mwalo pamoja na kuendesha shughuli za doria ili kupambana na uvuvi haramu.
Kwa upande mwingine akijibu swali la nyongeza kuhusu kuharibika kwa barabara ya Mikumi – Kilosa kusababisha kukatika kwa mawasiliano kutokana na mafuriko, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Kilimo katika kutafuta fedha kwa ajili ya kudhibiti mchanga unaoingia na kuziba mto.