Serikali imesema inafuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji wa mikopo kwa njia ya kidigitali iliyoidhinishwa na kwamba itakapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa matakwa ya leseni ya utoaji wa mikopo hiyo hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni watoa huduma husika.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Shally Raymond aliyetaka kufahamu wakati ambapo kampuni za simu zitalazimishwa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo, kwa kuwa kampuni za simu ndizo zinazoongoza kutoa mikopo kwa haraka bila kujaza fomu au chochote ambapo vijana na wajasiriamali wengi wakiwemo wakina mama huvutiwa nayo.
Dkt. Nchemba alisema, kwa mujibu wa sheria za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, hakuna kampuni ya simu iliyopewa leseni ya kutoa mikopo kwa wananchi kwa kuwa ili kampuni, taasisi au mtu binafsi aweze kutoa mikopo kwa wananchi anapaswa kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kukidhi matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha (The Banking and Financial Institutions Act, 2006) na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha (Microfinance Act, 2018).
Aliongeza kuwa, Kampuni za simu zinazotoa huduma za fedha zimepewa leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo kulingana na matwaka ya sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 (The National Payment Systems Act, 2015) pamoja na kanuni zake. Kampuni hizo zipo sita (6) ambazo ni: M-Pesa Limited, Honora Tanzania Mobile Solution Limited (Tigopesa), Airtel Money Tanzania Limited (Airtel Money), Viettel Ecommerce Limited (Halopesa), TTCL Pesa Limited (T-Pesa), na Azam Pesa Tanzania Limited (AzamPesa).
“Mikopo inayotolewa kwa wananchi kupitia simu za kiganjani hutolewa kwa ushirikiano kati ya taasisi zilizopewa leseni ya kutoa mikopo na kampuni za simu zilizopewa leseni ya mifumo ya malipo, ushirikiano huu unaainisha majukumu ya kila mtoa huduma ambapo taasisi zinazotoa mikopo hutoa mikopo hiyo kulingana na sheria na kanuni za leseni za utoaji mikopo huku kampuni za simu zikitoa mifumo, wateja na mwenendo wao wa kutumia huduma za kifedha” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba aliongeza kuwa mikopo yote hutolewa kupitia benki na watoa huduma ndogo za fedha ambapo inawafikia wananchi wote wenye uhitaji na wenye kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kutumia mifumo ya malipo ya kampuni za simu ambayo wateja wao wapo nchi nzima.
Alisema kuwa hatua hiyo imewasaidia wananchi kupata mikopo bila uhitaji wa kuwa na akaunti ya benki wala dhamana ya mkopo husika.