Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu wa malipo ya wananchi waliohamishwa katika eneo la Nyantwali ili kupisha hifadhi na mapito ya wanyama.
“Naomba muwe watulivu, tathmini ilikwishafanyika na sasa Serikali inakamilisha taratibu za mwisho za uhakiki ili kufanya malipo kwa wananchi wote.”
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Februari 26, 2024) alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Robert Maboto kuhusu malipo ya fidia kwa wakazi wa Nyatwali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Miembeni.
Waziri Mkuu amesema kumekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakitakiwa kulipwa fidia kwani baadhi yao wamekuwa si waaminifu kwa kuleta taarifa zisizo sahihi na wengine kuweka pingamizi juu ya utaratibu wa malipo.
Mapema, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji wa Misisi – Zanzibar ulioko kata ya Sazira ambao umegharimu sh. milioni 733 na hadi kufikia Januari, 2024 unahudumia wakazi 152,708 wa mjini Bunda.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), Bi. Esther Gilyoma alisema mradi huo umetokana na kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa chujio la kutibu na kusafisha maji Nyabehu ikiwa ni sehemu ya upanuzi wa mtandao wa huduma hiyo kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema kazi ya ujenzi ilihusisha tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 na maji hayo yanahudumia mitaa ya Nyasura ‘B’, Zanzibar na Misisi mjini Bunda.