Wabunge wameitaka serikali kuja na mpango mkakati wa kutoa ajira za kutosha katika kada za elimu na afya ili kukabiliana na uhaba wa watumishi nchini hali itakayoendana na utekelezaji wa miundombinu uliofanyika hivi karibuni.
Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka 2024/25, walisema sekta hizo zinahitaji ajira za kutosha.
Aidha, baada ya wabunge wanne kuchangia hoja ya ajira, Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amelijulisha Bunge kuwa usiku wa kuamkia jana Rais Samia Suluhu Hassan, alisikia kilio chao na kutoa kibali cha ajira 46,000 kwa kada mbalimbali.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, amesema uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na sekta ya afya vinatakiwa kuendana na ongezeko la watumishi kwa serikali kutoa ajira za kutosha ili majengo husika yaweze kutumika ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.
Amesema kwa sasa serikali ijikite zaidi kupeleka watumishi pamoja na vifaa tiba katika vituo vinavyojengwa, alitaja katika jimbo lake wana upungufu wa walimu shule 175, sekondari upungufu walimu 202, afya watumishi 175.
“Natambua kwamba kuna ujenzi wa madarasa, vituo vya afya pamoja na zahanati kote nchini, lakini jambo hili litakuwa na maana zaidi kama tunaongeza idadi ya madarasa, lazima iendane na idadi ya walimu kwani shida ya Watanzania sio majengo bali ni elimu na huduma bora za afya,” amesema Khenani.
Aidha, ametaja upungufu wa watumishi wengine wanaotegemewa zaidi katika maeneo husika ni pamoja na watumishi saba, watendaji 15 hali inayorudisha nyuma ukusanyaji mapato, watendaji wa vijiji ni 25.