Serikali mbili zinazohasimiana nchini Libya zinaratibu juhudi za kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko, Umoja wa Mataifa umesema.
Zaidi ya watu 5,300 walikufa baada ya mabwawa mawili kupasuka kusababisha mafuriko makubwa katika mji wa mashariki wa Derna.
Takribani watu 10,000 hawajulikani walipo, na makumi ya maelfu ya wengine wameyahama makazi yao.
Afisa wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa serikali zote mbili za mashariki na magharibi zimeomba msaada wa kimataifa na zinawasiliana.
“Serikali zote mbili zimewasiliana na jumuiya ya kimataifa kuomba huduma na usaidizi,” Tauhid Pasha, wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, alikiambia kipindi cha The World Tonight cha BBC Radio 4.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa [serikali ya magharibi] imetoa msaada wake kwetu na ombi lake kwa niaba ya nchi nzima na pia wanashirikiana na serikali ya mashariki,” alisema.
“Changamoto sasa ni jumuiya ya kimataifa kujibu ipasavyo mahitaji na maombi ya serikali,” aliongeza.
Bw Pasha alisema msaada unahitajika kuongezwa “haraka sana na kufanya hivyo tunahitaji pesa”.
Tangu kuangushwa kwa mtawala wa muda mrefu Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya imegawanyika kati ya serikali mbili zinazohasimiana na kuzama katika mzozo kati ya wanamgambo mbalimbali.
Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah anaongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa huko Tripoli, mji mkuu wa Libya, magharibi mwa nchi hiyo.
Osama Hamad, waziri mkuu wa mashariki, anaongoza utawala hasimu unaojulikana kama Baraza la Wawakilishi.
Hatahivyo, wengi wanahisi nguvu huko inashikiliwa na jenerali hodari wa kijeshi Jenerali Khalifa Haftar, anayeongoza Jeshi la Kitaifa la Libya, Jenerali Haftar alipokea ujumbe wa kijeshi wa Misri ambao ulikuja kutoa msaada baada ya maafa.