Serikali nyingi za Ulaya Jumatatu zilisema zinawaita mabalozi na wanadiplomasia wa Russia nchini mwao, kwa kile kinachoelezwa kuwa majadiliano, kufuatia kifo cha kiongozi wa upinzani wa nchio hiyo Alexei Navalny.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stephane Sejourne alisema katika ziara yake nchini Argentina kwamba balozi wa Russia mjini Paris ataitwa kwa maelezo, huku wizara ya mambo ya nje ya Norway ikitoa taarifa kwamba inamwita mwanadiplomasia wake mkuu wa Russia “kwa mazungumzo” kuhusu kifo cha Navalny.
“Katika mazungumzo hayo, maoni ya Norway yatatolewa kuhusu jukumu la serikali ya Russia katika kifo hicho na kuhusu umuhimu wa kuwezesha uchunguzi wa uwazi,” Norway ilisema, na kuongeza kuwa mkutano huo bado haujafanyika lakini ungefanyika hivi karibuni.
Kauli hizo zilifuatia taarifa nyingine kama hizo mapema Jumatatu, zilizotolewa na Finland, Ujerumani, Lithuania, Uhispania, Sweden na Uholanzi wakisema wamewaita wanadiplomasia kutoka balozi za Russia nchini mwao. London ilikuwa imefanya vivyo hivyo Ijumaa wiki jana, punde tu baada ya ripoti za kifo cha Navalney kuibuka.