Serikali ya Denmark iliwasilisha mswada siku ya Ijumaa ambao unaweza kusababisha marufuku ya kuchoma Quran hadharani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Lars Lokke Rasmussen, aliiambia redio ya Denmark kwamba hatua hiyo inatuma “ishara muhimu ya kisiasa” kwa ulimwengu wote.
Kuchoma Quran chini ya sheria mpya itakuwa ni kitendo cha kuadhibiwa kwa faini au kifungo cha hadi miaka miwili jela.
Peter Hummelgaard, waziri wa sheria, alieleza kuwa sheria inayopendekezwa inakusudiwa kuandikwa katika kanuni hiyo hiyo ambayo kwa sasa inapiga marufuku kunajisi bendera za nchi nyingine.
Sheria ya Denmark itakataza “kutendewa isivyofaa kwa vitu vyenye umuhimu wa kidini kwa jumuiya ya kidini”, alisema.
Hummelgaard, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, alisema kuwa mfululizo wa uchomaji moto wa hivi karibuni wa Qur’ani ulikuwa “kejeli zisizo na maana” zinazolenga kuchochea “mifarakano na chuki”, akiongeza kuwa usalama wa taifa ndio “msukumo” mkuu wa kupiga marufuku.
Mswada huo ungelifanya kuwa kosa la jinai kuchoma kitabu kitakatifu cha Waislamu, Biblia au Torati hadharani.
Bado haijafahamika ni lini pendekezo hilo litawasilishwa kwa Bunge la Denmark lenye viti 179.