Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf, Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa hati 8 za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya.
Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.