Ujerumani imemtaka balozi wa Chad mjini Berlin kuondoka nchini humo ndani ya kipindi cha masaa 48 yajayo ikijibu hatua kama hiyo iliyochukuliwa na taifa hilo la Afrika juma lililopita.
Taarifa fupi iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ujerumani imesema kuwa, balozi Mariam Ali Moussa, anapaswa kuondoka haraka nchini Ujerumani.
Wiki iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Chad ilitangaza kumkukuza nchini humo balozi wa Ujerumani kwa kile kilichoelezwa kuwa, mtazamo wake usio na adabu na kutoheshimu kanuni za kidiplomasia.
Chanzo cha serikali kililiambia Shirika la Habari la AFP, kwa sharti la kutotajwa jina, kwamba balozi wa Ujerumani nchini Chad Jan Christian Gordon Kricke, alionekana “kuingilia sana” utawala na mamlaka ya nchi na kutoa matamshi ya kuzusha mgawanyiko.
Baadhi ya duru zinasema kuwa kabla ya kufukuzwa nchini Chad, balozi huyo wa Ujerumani alikuwa ameonywa mara kadhaa, lakini hakurekebisha mwenendo wake huo.
Hata hivyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ujerumani imekanusha balozi wake huyo kutenda kosa lolote lile, na badala yake imesema, balozi Kricke alikuwa akitekeleza majukumu yake ipasavyo akiwa ameshiriki kwenye mazungumzo juu ya haki za binaadamu na kurejea haraka kwa utawala wa kiraia nchini humo.
Sasa Ujerumani nayo imechukua uamuzi wa kumfukuza nchini humo balozi wa Chad jambo ambalo bila shaka linaonyesha kuibuka mgogoro wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili.