Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Rais wake Mh. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuhakikisha Tanzania inazalisha wataalamu wenye viwango vinavyokubalika duniani kote. Kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) chuo cha MUST Kimeendelea kuboreshwa kupitia mradi huu wa kimkakati unaotarajiwa kugharimu dola za kimarekani 31.5 kwa kampasi zake zote mbili. Serikali inaendelea kuwekeza kwenye elimu hasa katika sayansi na teknolojia ndio lengo hasa ya kuanzisha mradi huu mkubwa.
Timu kutoka benki ya dunia iliyoambatana na wawakilishi kutoka wizara ya elimu ilifika MUST kuona maendeleo ya mradi huo.
Akiwakaribisha chuoni hapo, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Godliving Mtui alisema chuo cha MUST kimejipanga kisawasawa kukamilisha mradi huu kwa wakati.
Mratibu wa Mradi huo wa HEET Cornel Msemwa ameeleza utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kufuata taratibu na kanuni za Serikali na Benki Kuu ya Dunia. Mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa ni pamoja ufungaji wa miundo mbinu ya kidigitali, ununuzi wa magari na vitabu 7,861 na kutoa ufadhili wa masomo kwa wahadhiri 85. Kukamilika kwa majengo yanayojengwa kunatarajia kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.
Kwa upande wake mratibu wa Taifa wa mradi wa HEET Dkt Hosea amekipongeza chuo cha MUST kwa utekelezaji wa mradi huo hususani kwenye ujenzi na maeneo mengine ya mradi. Nae kiongozi wa msafara wa Benki ya Dunia, ndugu Roberta amesema kuwa nia ya ujio wao ni kujiridhisha kuhusu utekelezaji mradi huo na kukipongeza Chuo cha MUST kwa kasi nzuri ya utekelezaji wa mradi huo.
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Aloys Mvuma ameishukuru serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo utakaoleta mabadiliko kubwa chuoni hapo. Pia amewashukuru wawakilishi wa Benki ya Dunia kwa kufika chuoni na kwa maoni yao chanya kuhusu utekelezaji wa mradi huo.