Serikali iko mbioni kukamilisha Mradi wa Maji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 6.5 ambao umefikia asilimia 95 uliokuwa ukijengwa katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita Mkoani humo ambapo mpaka sasa mradi uko katika hatua za Majaribio hadi sasa.
Akizungumza na Millard ayo Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) Bw.Elenest Jackson amesema mradi huo unatarajia kuhudumia Maeneo mbalimbali ya Mji wa Katoro ikiwemo kata ya Nyamigota, Kata ya Buselesele na Kata ya Katoro ambapo wakazi wapatao Elfu 68 ni watanufaika na Mradi huo.
“Mradi huu ulianza mwanzoni mwa mwaka 2021 na kwa sasa hivi tuko kwenye hatua za Mwisho kabisa tunategemea kukamilka kwa mradi huu utaweza kunufaisha takribani watu elfu 68 kwa hatua hii kama mnavyoona tumeanza kuunganishia watu majumbani kwa ajili ya majaribio mpaka sasa tumeshaunganishia watu 10 mradi mpaka kukamilika unagalimu takribani bilioni 6.5 , ” Mhandisi Jacksoni.
Aidha Mhandisi Jackson amesema kwa sasa wameanza kuunganisha Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wananchi ambapo wananchi 10 tayari wamekwisha kuunganishwa na Mradi huo na tayari wameanza kunufaika nao.
Benjamine Jackson ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi kilimani iliyoko Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro amesema Mradi huo ni chachu ya kuondoa changamoto katika shule hiyo ambapo toka shule hiyo imeanzishwa haikuwai kupata Maji tofauti na Mradi huo uliokamilika.
Amesema Changamoto iliyokuwepo ilikuwa ni wanafunzi kukosa Maji ya kutumia nyakati za kufanya usafi Madarasani pamoja na maji ya kutumia kwenye vyoo vya shule hali ambayo ilikuwa ikiwapelekea kwenda kujisaidia nyumbani na wengine kupelekea utoro Mashuleni.
Wananchi pamoja na Wanafunzi wameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka katika kuhakikisha inakamilisha Mradi huo ambao ulikuwa umesubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Maeneo mbalimbali ya Mji wa Katoro Mkoani Geita.