BODI ya Sukari Tanzania imekanusha taarifa za kuchelewa kutoa vibali vya uagizaji wa sukari kwa kampuni za wazalishaji nchini, badala yake baadhi ya kampuni hizo zilichelewa zenyewe kuchukua vibali hivyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, kama njia ya kuelimisha jamii baada ya upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na baadhi ya wadau wa sukari nchini hapa.
“Napenda kuuhabarisha umma wa watanzania kuwa, si kweli kwamba wazalishaji wa sukari nchini walicheleweshwa kupewa vibali, isipokuwa wao ndiyo walichelewa kuchukua vibali,” Alisema Profesa Bengesi.
Aidha Profesa Bengesi alisema wazalishaji walipewa vibali kabla ya kampuni za wafanyabiashara wanazoziita za “vocha” zilizopewa vibali baada ya kuona mwenendo wa uingizaji wa sukari wa kampuni za wazalishaji kuwa sio mzuri.
Profesa Bengesi alisisitiza kuwa kitendo cha wadau kusema Bodi ilitoa vibali vya sukari kwa wafanyabiashara kwanza kabla ya kuwapa wazalishaji, ni upotoshaji wa makusudi ili kuzua taharuki kwa Watanzania.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Sukari inaonyesha kampuni za wazalishaji zilipewa vibali vyake mwanzoni mwa mwezi Januari, wakati kampuni za wafanyabiashara zilipewa vibali hivyo mwishoni mwa mwezi January na mwezi Aprili.