Serikali imeridhia ombi la kujengwa Mnara wa Sokoine katika eneo la Dakawa mkoani Morogoro, eneo alilopata ajali na kufariki dunia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametangaza kuridhia kujengwa kwa Mnara huo wakati akifungua mdahalo wa Kumbukizi ya Hayati Sokoine kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoani humo.
Dkt. Mpango ameridhia ombi hilo ambalo lililotolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Aidha, Makamu wa Rais amemuelekeza Prof. Ndalichako kushughulikia mchakato utakaofanikisha kujengwa kwa Mnara huo wa Sokoine aliyefariki dunia mwezi Aprili mwaka 1984.