Serikali imesema nchi yetu inaendeshwa kwa kuheshimu utawala wa Sheria na kwamba mamlaka ya kutafsiri sheria yamekabidhiwa kikatiba kwa mhimili wa Mahakama; hivyo imeshauri wafugaji ambao wanaona hawakutendewa haki pale ambapo mifugo yao ilikamatwa kwa kuvunja sheria ya kuingia kwenye hifadhi za taifa au kwenye mapori ya akiba wakakate rufaa kwenye chombo cha kutafsiri sheria ambacho ni mahakama.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula akijibu swali la Mhe. Emannuel Lekshon Shangai Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro ambaye alitaka kujua Sheria inayoruhusu watumishi wa TANAPA, TAWA na NCAA kutoza faini ya mifugo ya Shilingi 100, 0000/= pindi iingiapo Hifadhini.
Aidha Mhe. Kitandula alisema kwamba Taasisi za Uhifadhi za TANAPA, NCAA na TAWA zinaongozwa na Sheria mahsusi za kusimamia rasilimali za wanyamapori.
“Mathalan, Sheria ya TANAPA Sura 282 Kifungu cha 28(1)(a) kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2003 ambayo imeongeza Kifungu 20A cha Sheria hiyo kwa kuwapa mamlaka watumishi wa TANAPA kutoza faini isiyozidi Shilingi 100,000/= kwa kila kosa pale mkosaji anapokiri na kukubali kwa maandishi kulipa faini kwa kosa husika” aliongeza Mhe. Kitandula.
Vilevile kifungu cha 116 cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura ya 283 hutumika katika kutoza faini pindi mifugo inapoingizwa kinyume cha Sheria ndani ya mapori ya akiba.
Mhe. Kitandula alifafanua kuwa kifungu hiki kimebainisha utaratibu wa kulipa faini ambapo mkosaji atalipa faini mara baada ya kukubali na kukiri kosa.
Aidha, Sheria imeelekeza kuwa kiwango cha faini hakitapungua Shilingi 200,000/= na hakitazidi Shilingi 10,000,000/=.
Mhe. Kitandula alitoa rai kuwa Serikali itaendelea kuhifadhi na kusimamia rasilimali za wanyamapori kwa kushirikiana na jamii.
“Hivyo, tunawaomba watoe ushirikiano katika kufanikisha jukumu hilo na kuwasihi wazingatie Sheria ili kuepusha migongano isiyo ya lazima baina yao na hifadhi.” Mhe. Kitandula amesisitiza.