Kampuni ya kutengeneza na kusambaza mbolea ya YARA imezindua programu maalumu iitwayo ‘YaraConnect APP’ ikiwa na malengo ya kutoa elimu ya kitaalmu kuhusu kilimo kwa wateja wao watakaojisajili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo alisema uzinduzi wa YaraConnect ni moja ya malengo yao katika kubuni mbinu sahihi za kitaalamu katika kilimo ikiwemo za njia ya kidijitali.
Alisema Yara ni kampuni inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa mbolea nchini Tanzania kwa takribani miaka 15 sasa ikiwa kampuni inayoongoza duniani katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea ,utunzaji wa mazingira na kutoa suluhisho la kitaaluma kuhusu uzalishaji wa mazao mbali mbali.
“Hii ni App mpya kabisa itakayopatikana kwa kupitia simu za smart na inalenga wauzaji na wasambazaji wa bidhaa za Yara, watumiaji wa simu za android wataweza kupakua App hii kupitia Playstore na wale wa iOS (Iphone) watapakua kupitia Appstore”, Odhiambo
Aidha alisema wasambazaji pia watajifunza kupitia video za maarifa zipatikanazo ndani ya App na kujua maswali yanayoulizwa sana na wakulima wa eneo husika ambapo watumiaji watapata nafasi ya kupata msaada wa kitaalamu kuhusu lishe linganifu kwa mimea kupitia App hiyo.
“Napenda kuwafahamisha kuwa tutazindua App hii rasmi mwezi huu katika mikoa saba ya Tanzania bara ambayo ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Njombe, Mbeya, Iringa na Morogoro. Hivyo tunawakaribisha na kuwataarifu wasambazaji wa pembejeo kwa maeneo husika yakuwa hafla hii siyo ya kukosa ili kuboresha huduma zao na kunufaika kipekee.
“Yara inatoa wito kwa wasambazaji wote wa bidhaa zetu wachangamkie fursa hii na tunaahidi kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kuendelea kubuni mbinu nyingine za kidijitali zaidi ili kuhakikisha wadau wetu wanapata mafanikio mengi.
“Shughuli hii maalumu ya leo inatufanya Yara tuendelee kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kilimo, mazingira na lishe hapa nchini Tanzania na duniani”, aliongeza Bwana Winstone.
Wateja na wadau wa Yara wanaweza pia kupata taarifa zaidi kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram, facebook, twitter na youtube kwa kutumia jina yaratanzania.