Serikali imetoa maelekezo kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) kuhakikisha inakagua viwanda 12 vya kuzalisha bidhaa za afya ili kuona kama vinakidhi viwango na hatimaye litolewe tamko la kuzuia aina nane ya dawa za vidonge kuagizwa kutoka nje ili dawa hizo ziwe zinanuliliwa katika viwanda vya ndani.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi wakati wa kikao maalum kilichoandaliwa na Bohari ya Dawa(MSD)kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika na uzalishaji dawa na vifaa tiba nchini kwa lengo la kuangalia namna ya kuongeza uzalishaji na kupunguza ununuaji bidhaa za afya nje ya nchi.
Amesema katika kuhakikisha Serikali inapunguza uagizaji dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi kumekuwa na hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya ili dawa ziwe zinanunuliwa nchini badala ya kuagiza nje.
Amefafanua dhamira ya Serikali ni kuhakikisha jambo hilo la uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya nchini linafanikiwa huku akifafanua tayari kuna viwanda 12 ambavyo TMDA inatakiwa kuvikagua na hatimaye vianze kuzalisha na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya.
“Tayari Serikali imetoa maelekezo kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) kufanya uchambuzi wa bidhaa zinazozalishwa katika viwanda 12 .Lengo ni kuangalia ubora wa viwanda hivyo iwapo vinakidhi viwango vinavyotakiwa.
“Binafsi nimetembelea viwanda hivyo na nimejiridhisha na mazingira yake ambayo hayana tofauti na viwanda vya nje.Hivyo TMDA tunaielekeza ikakague viwanda hivyo na baada ya taarifa yao Serikali itatoa tamko kuzuia uagizaji dawa za vidonge ambavyo vitakuwa vinazalishwa katika viwanda hivyo.”
Aidha amesema Serikali inatambua vita iliyopo katika kufanikisha ujenzi wa viwanda lakini kwa mikakati iliyopo lazima dhamira ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba inatekelezwa na hiyo inatokana na hatua mbalimbali ambazo Serikali inaendelea kuchukua.
“Ukweli kuna viwanda ambavyo tulikuwa tunanunua bidhaa za afya kwao, hivyo kuwa na viwanda vyetu hao hawawezi kukubali lakini changamoto hiyo tutakabiliana nayo.Tunaka kuona viwanda vya ndani vinapewa nafasi kubwa na kuwahakikisha soko la uhakika.”
Pia Msasi amesema hivi karibuni Serikali imeridhia mkataba wa African Medicines Agency(AMA) wenye lengo la kulinda bidhaa zinazoingia Afrika na viwanda vya ndani vitasaidia dawa na kuuza Afrika.
Kuhusu mkutano wa wadau , Msasi amesema utasaidia kuibua changamoto ambazo Serikali itazifanyia kazi ili kuboresha uzalishaji wa ndani unakuwa na uagizaji kutoka nje ya nchi unaoungua ili kufikia mkakati uliopangwa wa mwaka 2030.
Ametoa mfano kuwa tayari Serikali imetoa zuio la kununua maji dawa kutoka nje ya nchi kwani tayari kuna viwanda ambavyo vinafanya uzalishaji wa maji dawa ambapo chupa moja ya maji inanunuliwa kwa Sh.700 na baada ya kuanza kununua ndani mzalishaji wan je aliyekuwa anauza kwa Sh.700 ameshusha bei hadi Sh.500.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Bohari ya Dawa(MSD) Leopold Shayo amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kununua bidhaa za afya kutoka nje ya nchi.
“Sasa tumekuwa na viwanda vya uzalishaji wa maji dawa na tunanunua maji hayo hapa hapa nchini, kinachotokea wale waliokuwa wanatuuzia mwanzoni wameshusha bei.
Akizungumzia bajeti ya dawa amesema MSD imekuwa ikitumia Sh.bilioni 590 kwa mwaka kununua dawa ambazo ni sawa na asilimia 80 ambayo ni sawa na Sh.bilioni 300 ambazo zingetumiwa na wazalishaji wa ndani badala ya kuzipeleka nje ya nchi.
Kuhusu bei ya dawa kwa wazalishaji wa ndani amesema kuna mambo mawili ambapo la kwanza inatokana na wazalishaji wa ndani kuwa wachache na ushindani hauko mkubwa kati yao.
“Kwa hiyo watataka kuweka kiwango ambacho hakitakuwa kikubwa sana katika kufidia gharama ambazo wamezitumia kuanzisha viwanda hivi. Nadhana itafika hatua fulani watakuwa wameshafikia malengo na bei zitashuka zaidi.
“Pia bidhaa za afya ambazo tunatumia katika kuzalisha hizi bidhaa za mwisho inawezekana bado hawajapata soko ambalo ni la uhalisia gharama zinaweza kuwa bado kwenye uagizaji
“Vile vile wazalishaji wa ndani kwa mfano kama ni wakulima ambao wanatengeneza bidhaa fulani au vitu fulani bado hawajapata changamoto ya kuweza kujua fursa ya uuzaji wa bidhaa zao ambao utaongeza uzalishaji.”