Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,serikali wilayani Njombe imewaonya waandikishaji wa vituo 227 vya uchaguzi waliokula kiapo Cha utii na Uadilifu kutotoa siri za mchakato huo kwani ni kinyume cha sheria na kanuni za uchaguzi.
Onyo hilo limetolewa na mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe George Makacha wakati akiwaapisha waandikishaji hao katika ngazi za vijiji na Kata,zoezi lililofanyika katika kata ya Mtwango wilayani humo.
“Yale utakayoyajua hupaswi kumwambia mtu yeyote yule kwasababu utakayoyajua na kuanza kuzungumza huko tutakuwajibisha kwa mujibu wa kiapo chako ndio maana tunaapa kabla na sio ninaongea kwa maana ya kutisha ila ni kwasababu kazi hii ni ya siri”Makacha
Msimamizi msaidizi wa uchaguzi na kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe CPA Asha Msangi Amesema hakuna kumuacha mwananchi yeyote mwenye sifa ya kuandikishwa katika kipindi cha siku kumi cha uandikishaji.
“Tuna kata kumi na mbili kwenye halmashauri yetu na tunategemea kuandikisha wapiga kura wasiopungua elfu hamsini na nne na zoezi letu la kuandikisha litaanza tarehe kumi na moja na kukamilika tarehe ishirini ya mwezi wa kumi ambapo vituo vya kuandikisha vitafunguliwa kuanzia saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili kamili jioni kwa siku zote kumi,mwanamnchi anapaswa kwenda kujiandikisha akiwa na majina yake matatu na mwandikishaji atamuuliza majina yake matatu,jinsia yake,umri wake na mwisho ataweka sahihi kwenye daftari la uandikishaji”amesema Asha Msangi
Baadhi ya waandikishaji waliokula kiapo na mafunzo ya kwenda kutekeleza zoezi hilo akiwemo Wema Chilonwa na Andrea Mara wameahidi kwenda kutunza siri za viapo vyao na kwamba watafanyakazi ya kuwaandikisha wananchi kwa kadri ya uwezo wao.
“Tumejiandaa vizuri kuhamasisha wananchi kwa ajili ya kujiandikisha kwa ajili ya kuchagua viongozi watakaofanya kazi kwa miaka mitano ili kuleta maendeleo kwenye vijiji na vitongoji kwa ujumla lakini pia tumepokea maelekezo ya namna ya kuandikisha wakazi”amesema Wema Chilonwa