Serikali kupitia Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imesema inaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ,kutoa elimu kwa jamii na kuweka mikakati thabiti ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko katika jamii.
Hayo amesemwa leo Disemba 14, 2022 na Dkt. James Kengia alipozungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais –TAMISEMI katika kikao kazi cha Tathmini ya Programu ya utoaji wa Elimu ya Afya na Ushirikishwaji wa Jamii katika Majanga mbalimbali ya magonjwa ya mlipuko kilichofanyika Mkoani Tanga.
Dkt. Kengia amesema lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo washiriki, kufanya tathmini,kubaini changamoto pamoja na kuweka mikakati ya namna bora ya kukudhibiti na majanga yanayosababishwa na magonjwa ya mlipuko.
“Nitoe rai kwa wataalam wa afya kwa ngazi ya jamii kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi ili mwananchi aweze kujikinga na magonjwa hayo, katika Ugonjwa wa UVIKO-19 tulishirikiana sana na viongozi wa dini katika kutoa elimu ya tahadhari, tuendelee kushirikiana nao ili tuwe na uwelewa wa pamoja” amesema Dkt. Kengia
Ameendelea kusema Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha miundombinu ya kutoa huduma za afya, kununua vifaa tiba pamoja na kuendelea kuajiri wataalam wa afya ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Afya Idara ya Kinga Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Bw. John Yuda amesema, Serikali inawataalamu ambao wanafanya utafiti katika kutafuta kinga na tiba sahihi ya magonjwa ya mlipuko ili kudhibiti maambukizi katika Jamii hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwasikiliza wataalamu wa afya kwa kuchukua tahadhari na kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa la Ebola ambao upo katika nchi jirani.
Naye mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Chipole Mpelembe amesema mfunzo hayo ya siku tatu yatasaidia kuongeza weledi na mbinu bora za kuongeza uwajibikaji katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na waratibu afya jamii kutoka mikoa 11 iliopo katika hatari yakupata ungonjwa wa Ebola, wadau wa maendeleo na watafiti.