Katika jitihada za kuendelea kulipa hadhi Jiji la Dodoma ambalo kwa sasa Ofisi nyingi za Serikali zimehamia huko, ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia aingie madarakani Barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka KM 699.625 mwaka 2020/21 hadi KM 1,925.084 sawa na ongezeko la 175.16% kwa mwaka.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe amesema ongezeko la bajeti limechangia kuimarika kwa hali ya mtandao wa barabara ambapo Barabara zenye hali ya wastani zimeongezeka kutoka KM 2,098.875 mwaka 2020/21 hadi KM 2,755.844 mwaka 2022/23 wakati Barabara zenye hali mbaya zimepungua kutoka KM 4,197.75 mwaka 2020/21 hadi KM 2,860.92, pia matengenezo ya mtandao wa Barabara yameongezeka kutoka KM 1.5 mwaka 2022/21 hadi KM 32.41 mwaka 2022/23 kwa Barabara za lami.
“Katika utekelezaji wa miradi ya Barabara kwa mwaka 2021/2022 jumla ya Tsh. Bil. 55.60 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo na ukarabati, ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na mwaka wa fedha 2022/23, TARURA Mkoa wa Dodoma imetengewa Tsh. Bilioni 52.16, uboreshaji wa miundombinu umesaidia kutatua shida za usafirishaji wa mazao, Watu na bidhaa na kusaidia kuongeza pato la Taifa na jamii kwa ujumla.”
“Ujenzi wa vivuko katika maeneo mbalimbali hususani madaraja umepunguza tatizo la usafiri hasa katika maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa hayafikiki kirahisi, kuongezeka kwa Bajeti kumeongeza Madaraja kutoka mawili mwaka 2020/21 mpaka madaraja 6 mwaka 2022/23″
“Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa Waziri Mkuu (KM 2) kwa gharama ya Sh bilioni3, ujenzi wa Barabara eneo la Nzuguni (Nanenane) KM 1.5 kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 na Barabara ya kisasa KM 1.5 kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 628.69, Barabara ya Bima/Mahakamani yenye urefu wa KM 2.2 kwa gharama ya Sh bilioni 2.5”