Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa tathmini ya athari ya miundombinu ya barabara nchini imebaini hadi kufikia jana Aprili 14, 2024 kuwa Wizara ya Ujenzi inahitaji kiasi cha Shilingi Bilioni 500 ili kuwezesha urejeshaji miundombinu ya barabara na madaraja katika hali yake ya kawaida katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-nino.
Bashungwa amesema hayo Bungeni Aprili 15, 2024 akijibu hoja mbalimbali za waheshimiwa wabunge wakati Bunge likijadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
“Wakati wa Bunge la mwezi wa pili tulifanya tathimini ya uharibifu wa miundombinu na hasara ilikuwa ni Bilioni 200, lakini mpaka jana miundombinu mingi imeharibika na ili tuweze kuirudisha tunahitaji Bilioni 500 (nusu Trilioni)”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa kiasi hicho cha fedha kinachohitajika ndicho kingeweza kupelekwa kwenye miradi ya barabara iliyopo katika hatua mbalimbali za ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ambazo zimeshasainiwa na zile ambazo zipo katika hatua za manunuzi.
“Kutokana changamoto ya mvua za El-Nino zinazoendelea kunyesha kupita kiasi, Wizara italazimika kujipanga upya kurejesha miundombinu hiyo ili kuhakikisha watanzania wanaendelea kuwa na mawasiliano ya barabara huku tukiendelea na mkakati wa kudumu wa kuzijenga kwa kiwango cha lami”, amefafanua Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa kila mwaka Serikali inatumia takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 550 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara za kiwango cha changarawe hapa nchini.
Vilevile, Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TANROADS na TARURA kuendelea kuweka jitihada za kurudisha mawasiliano pale yanapoharibika.
Kuhusu utekelezaji wa miradi hapa nchini, Bashugwa ameleeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa barabara 25 kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 1,198.5 na madaraja makubwa nane.