Israel ilikabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa siku ya Jumanne kukubali kusitisha mapigano na Hamas, huku ikipanga uvamizi katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza ambako zaidi ya Wapalestina milioni moja wamenaswa.
Mkurugenzi wa CIA William Burns alitarajiwa mjini Cairo siku ya Jumanne kwa duru mpya ya mazungumzo juu ya upatanishi wa usitishaji mapigano unaosimamiwa na Qatar ambao ungesimamisha mapigano kwa muda badala ya Hamas kuwaachia huru mateka.
Ziara yake iliyopangwa inakuja baada ya Washington na Umoja wa Mataifa kuionya Israel dhidi ya kufanya mashambulizi ya ardhini mjini Rafah bila mpango wa kuwalinda raia, ambao wanasema hawana pa kwenda.
“Popote tunapoenda kuna mashambulizi ya mabomu, mashahidi na kujeruhiwa,” alisema Iman Dergham, mwanamke wa Kipalestina aliyekimbia makazi yake.