MSF inasema hali hii imechangiwa na utovu wa usalama Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo ambapo, watu wenye silaha wameendelea kuwavamia watu, kuwauwa na kuwateka.
Mpaka sasa, Shirika hilo linasema limewatibu zaidi ya watoto Laki Moja na Elfu Sabini, wanaosumbuliwa na utapiamlo na wengine zaidi ya Elfu 32 wamelazwa hospitalini, wakiwa na hali mbaya.
Utovu wa usalama unasababisha wakaazi wa Kaskazini mwa Nigeria, kuishi maisha magumu kwa sababu hawawezi kujihusisha na shughuli za kiuchumi na sasa MSF inataka Umoja wa Mataifa na watoa misaada wa kimataifa kutambua hali hiyo na kuchukua hatua haraka.
Tangu mwaka 2009 mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitokeza kuwasaidia watu zaidi ya Milioni 2 waliokimbia makaazi yao, lakini kuna uhaba mkubwa wa mahitaji ya kibinadamu hasa chakula, dawa, maji safi na makaazi.