Shirika la kimataifa la Save the Children na washirika wake wamesema kuwa, wameunganisha watoto 7,000 na familia zao tangu 2017, na kuwawezesha kujenga upya maisha yao baada ya kutenganishwa na migogoro.
Shirika hilo la hisani limesema hayo katika taarifa yake kuwa limekuwa likitumia jukwaa la programu huria linalojulikana kama Child Protection Information Management System Plus (CPIMS+) kuwaunganisha watoto na familia zao nchini humo kwa miaka tisa.
Kupitia programu hiyo ambayo inajumuisha programu ya simu na uwezo wa nje ya mtandao, hivi karibuni wafanyakazi wa Save the Children walifanikiwa kuwakutanisha Simon, 13, na kaka yake mtu mzima Samuel baada ya kutengana na familia kwa miezi mitatu, na hivyo kufanya jumla ya watoto waliounganishwa na familia zao kupitia mpango huo wa Save the Children huko Sudan Kusini kufikia watoto 7,000 tangu mwaka 2017
Kwa mujibu wa hifadhidata ya CPIMS+, karibu watoto 20,000 waliotenganishwa na familia zao au waliopotea wamesajiliwa katika maneo tofauti ya Sudan Kusini katika kipindi cha miaka tisa iliyopita kutokana na migogoro ya ndani ya nchi hiyo na kutoka nchi jirani ya Sudan.
Katika taarifa yake hiyo, shirika hilo limesema: Watoto waliotenganishwa na familia zao na wasio na walezi wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na vitendo vya kiatili, unyanyasaji na unyonyaji, jambo ambalo linaufanya wajibu wa kuwarejesha kwa wazazi wao kuwa kipaumbele cha dharura kwa kila mtu.
Taarira hiyo imetolewa katika hali ambayo kwenye ripoti yake ya mwezi Julai mwaka huu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema kuwa, watu kutoka familia 38,697 wameripotiwa kuingia Sudan Kusini tangu mapigano baina ya majenerali wa kijeshi yalipoanza katika nchi jirani ya Sudan mwezi Aprili mwaka huu, na kuzidi kuitia kwenye matatizo Sudan Kusini.