Shirika lisilo la Kiserikali la “Utu Kwanza” limeandaa mbio za Utu Kwanza Run kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasaidia wananchi mbalimbali walio katika nafasi finyu ya kupata huduma ya msaada wa kisheria ikiwemo huduma ya kwanza ya kisheria (first response) hususan kwa wale walioko magerezani na mahakamani pamoja na familia zao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo tarehe 10 Septemba, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa shirika hilo Wakili Shehzada Walli amesema, mbio hizo zinatatajiwa kufanyika Septemba 10, 2023 jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Leaders -Kinondoni na kutoa wito wito kwa kila mmoja kuunga mkono Utu Kwanza Run katika kufanikisha mbio hizo.
“Ili kuweza kufanikisha tuliyoazimia kama taasisi ya Utu Kwanza ikiwemo kutoa msaada wa kisheria pamoja na huduma ya kwanza ya kisheria (first response) kuwasaidia wananchi mbalimbali hususan walioko mahakamani, tumeamua kuja na mbio maalum zinazoitwa Utu Kwanza Run kwa lengo la kuchangisha fedha I’ll kufanikisha azma hiyo ” alisema Wakili Walli na kuongeza
“Utu Kwanza Run itafanyika Septemba 10, 2023 ambapo katika siku hiyo kuanzia saa 4a asubuhi hadi saa 8 mchana kutakuwa na dawati la kutoa msaada wa kisheria hususan wale walioko magerezani. Tunawaomba familia zao waweze kujumuika nasi siku hii.”
Akielezea mpangilio wa mbio hizo, Wakili Walli amesema, kutakuwa na kilometa 5 na 10 hadi kilometa 60 kwa wanaokimbia na kutembea, kwa upande wa waendesha baiskeli itakuwa ni kilometa 25 hadi kilometa 60 .
Wakili Walli ameeleza kuwa huduma ya kwanza ya msaada wa kisheria na msaada wa kisheria kwa ujumla watakaoutoa itatolewa kwa kuanzia katika Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya na kubainisha kuwa katika mahakama hizo wengi wao wako katika nafasi finyu sana ya kupata msaada wa kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amelipongeza shirika hilo kwa kuja na ubunifu katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ikiwemo kuja na mbinu tofauti.
“Kitu wanachokwenda kukifanya taasisi ya Utu Kwanza kutoa huduma ya kwanza ya msaada wa kisheria ni cha kipekee na cha kupongeza, kitu ambacho ni tofauti na wadau wengine wanaotoa msaada wa kisheria kwani wamewekeza katika makosa ya jinai, na jambo hili limekuja katika muda mwafaka wa mabadiliko ya mfumo wa haki jinai” alisema Akili Masawe
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Moil Altaf Mansoor amesema, hatua ya taasisi ya Utu Kwanza kuanzisha mradi wa Dawati la Msaada wa Kisheria (Legal Aid Desk Project) inalenga katika kuhakikisha utu na haki ya mtu inapatikana na ni miongoni mwa jambo muhimu sana kwa nchi.
“Tunahitajika kuunga mkono hatua za kupatikana haki na utu, kwa kuwa bila kuhudumia jamii sidhani kama maisha yatakuwa yana maana, tuihudumie jamii ili kuyapa thamani na maana maisha yetu”
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Baiskeli ya Twende Butiama, Gabriel Landa amethibitisha klabu yake kushiriki katika mbio hizo lengo likiwa ni kuhamasisha na kuunga mkono utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa watu wanaokosa huduma hiyo na kuongeza kuwa jambo hilo ni la kizalendo.
“Utu Kwanza” ni Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) lililosajiliwa chini ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. NGO ilianza shughuli zake mwaka wa 2019 na inafanya kazi katika kutafuta kuhifadhi utu na heshima ya binadamu kwa kusaidia hasa wafungwa wote wawili, waliohukumiwa na wasio na hatia, pamoja na familia zao. Dhamira ya shirika hili ni kutetea utu kwa kuimarisha ubora wa maisha ya jumuiya na kutoa uhakikisho kupitia usalama na uthabiti.