Shirika la sayansi Duniani yaani World Organization for Science literacy lenye makao yake makuu katika mji wa Beijing nchini China limesema limeingia makubaliano na shule ya Kadama English Medium iliyoko Kata ya Buseresere Wilaya ya Chato Mkoani Geita kuanzisha kituo cha Sayansi katika shule hiyo kwa ajili ya kufundisha wanafunzi njia rahisi za kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo kwa kutumia vifaa vinavyo patikana katika mazingira yao.
Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Tanzania Dr. Wilson Stephen akizungumza katika mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Kadama Agosti 19 2023 amesema kituo hicho ni mkakati wa kufundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa vitendo ili kukabiliana na tatizo la upungu wa vifaa vya maabara ambalo linasumbua nchi nyingi za kiafrika.
Amesema kuwa mbinu hizo zinatumika sana na nchi zilizo endelea kisayansi kama Australia na China ambapo mwanafunzi anajifunzi zaidi kwa vitendo kuliko nadharia na hivyo kuvutiwa na masomo ya sayansi.
Dr.Stephen amesema katika Mkoa wa Geita kituo kitakuwa shule ya Kadama na wanatarajia kufikia shule nyingi zaidi kwa ajili ya kuandaa walimu na wanafunzi wengi zaidi ili kuodoka tatizo la maabara na uhaba wa vifaa vya maabara.
Mkurugenzi wa shule hiyo Leticia Pastory amesema kuwa shirika hilo limefikia uamuzi huo wa kuanzisha kituo cha sayansi kwenye shukle hiyo baada ya kuvutiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wengi wanaomaliza katika shule hiyo kusoma masomo ya sayansi.