Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa Mkoa kidato cha nne uliofanyika kati ya Julai 15 na Agosti 1, 2024, shule za Serikali zimeendelea kushika nafasi za chini katika mikoa mitano ya kanda ya Ziwa.
Akitangaza matokeo hayo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Emily Kasagala alibainisha kuwa Mkoa wa Mwanza umeongoza kwa kuwa na GPA ya 3.72, sawa na asilimia 86.13%, huku Shule za watu binafsi zikiwa zimefanya vizuri zaidi ikilinganishwa na shule za Serikali.
Shule za Serikali zimeonekana kushika nafasi za chini zaidi, huku Geita Sekondari ikitajwa kama shule iliyofanya vizuri zaidi miongoni mwa shule za serikali. Kwa upande mwingine, shule zilizofanya vibaya zaidi ni pamoja na Lukoma kutoka Bukoba, Murugwanza kutoka Ngara, na Profesa Joyce Ndalichako kutoka Muleba. Aidha masomo ya Hesabu, Historia, na Civics yameonekana kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza Martin Nkwabi amewataka wakuu wa Shule za Serikali kuhakikisha wanatafuta sababu za matokeo duni na kuchukua hatua za haraka kurekebisha ili kuboresha matokeo ya wanafunzi wao katika siku zijazo.
Hatua hii inalenga kuondoa kabisa matokeo mabaya katika Shule hizo na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora zaidi.