Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imezifunga shule zote kuanzia awali hadi kidato cha Sita kwa muda wa mwezi mmoja, ikiwa ni hatua za awali za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Waziri Mkuu ameyabainisha hayo leo Machi 17, 2020, wakati akitoa tamko rasmi la Serikali na kuitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kusimamia mipaka yote na kwamba watu wote wanaoingia nchini waingie kupitia mipaka ambayo ni rasmi.
“Tumefunga Shule zote za Awali hadi Kidato cha Sita na zitafungwa kwa muda wa siku 30 kuanzia leo, Wizara itafanya marekebisho ya ratiba ya mtihani wa kidato cha sita, tumesitisha pia michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama Ligi Kuu, Michezo yote ya shule, UMISETA, UMITASHUMITA,” Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu akatoa agizo kwa Wizara ya Afya,“Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (Hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida, Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara ambao wanapandisha bei”.