Akitangaza kifo cha Jenerali Ogolla rais Ruto amesema kutakuwa na siku tatu za maombolezo kuanzia Ijumaa tarehe 19 Aprili ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwa kipindi hicho .
Helikopta ya kijeshi ya Kenya iliyokuwa imembeba Mkuu huyo wa Majeshi Francis Ogolla ilianguka katika mpaka wa Kaben-Cheptule kati ya Elgeyo Marakwet na Kaunti ya Pokot Magharibi katika eneo la magharibi nchini humo, takriban kilomita 400 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Nairobi.
Maafisa hao walikuwa wamesafiri hadi eneo la kaskazini mwa Kenya ambalo limekuwa likikumbwa na visa vya wizi wa mifugo.
Rais Ruto amemtaja Jenerali Ogolla kama afisa shupavu aliyefariki akiwa kazini.
Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi mnamo Aprili 2023.
Alichukua nafasi kutoka kwa Jenerali Robert Kibochi ambaye aliondoka baada ya kutimiza umri miaka 62.
Kabla ya uteuzi huo Jenerali Ogolla alikuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.