Siku tisa baada ya maafa ya tetemeko la ardhi Uturuki, wanawake watatu na watoto wawili wamepatikana wakiwa hai.
Melike Imamoglu mwenye umri wa miaka 42 na Cemile Kekec mwenye umri wa miaka 74 walitolewa kwenye vifusi na waokoaji katika mji wa Kahramanmaras nchini Uturuki.
Uokoaji wao ulikuja wakati wafanyikazi walielekeza umakini wao katika kusafisha miji iliyoharibiwa na matetemeko ya ardhi ya Februari.
Mamilioni ya watu kote Syria na Uturuki wanaishi katika kambi za muda na wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Video ya uokoaji iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii na Meya wa Darica, Muzaffer Biyik, ilionyesha wafanyakazi wakipiga makofi na kukumbatiana huku Bi Kekec akiingizwa kwenye gari la wagonjwa.
Huko Antakya-mji mwingine wa Uturuki ulioathiriwa vibaya na matetemeko ya ardhi – vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba mama na watoto wake wawili walitolewa wakiwa hai kwenye vifusi.
Siku kumi baada ya maafa, inakuwa vigumu kupata manusura wa tetemeko hilo. Idadi ya vifo vilivyojumuishwa sasa imepita 41,000.