Siku ya Kimataifa ya Wanawake, kampeni ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha juhudi za kuleta usawa wa kijinsia duniani kote, mwaka huu inaadhimishwa kesho Ijumaa, kaulimbiu ikiwa ni “Wekeza kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo .”
Nia yake ni kuwezesha uthabiti wa kiuchumi wa wanawake, ambako kunaweza kuwa ni hatua chanya kufikia juhudi za usawa.
Duniani kote, haki za wanawake zinazidi kutishiwa, au kupiga hatua nyuma, hata katika maeneo ambayo viongozi walidhani wamepiga hatua chanya.
Kulingana na na shirika la wanawake la UN Women, mwanamke mmoja kati ya 10 hivi leo anaishi katika umaskini uliokithiri kulingana na Jemimah Njuki, mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wa kiuchumi katika shirika la wanawake la Umoja wa Mataifa
Tafiti pia zinaonyesha kuwa takribani wanawake na wasichana milioni 340, asilimia 8 ya wanawake duniani, hawatakuwa wameondoka kwenye umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030, iwapo mienendo iliyopo sasa itaendelea.