Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amepiga marufuku Wananchi kukatiwa maji Wikiendi na Sikukuu huku akiwaagiza pia Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji kuhakikisha maunganisho ya maji kwa Wateja wapya yanafanyika ndani ya siku saba.
Akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Aweso amesema “ Wizara ya Maji imepanga kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Mijini kwa kuhakikisha maunganisho kwa Wateja yanafanyika ndani ya siku 7 na mkakati wa Wizara ya Maji ni kuboresha huduma kwa Wateja, tumeona baadhi ya Mamlaka Mwananchi anataka kuunganishiwa huduma ya maji lakini zinatumia wakati mwingine zaidi ya miezi miwili hadi tatu, nataka niwaambie Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji kipimo cha maunganisho ya maji kwa Wateja ni ndani ya siku 7”
“Kipimo cha Watendaji wa Wizara ya Maji naomba mnisikie ni upotevu wa maji, haiwezekani leo Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu unakwenda kuitembelea Mamlaka ya Maji anakwambia upotevu wa maji ni asilimia 45%, hatuwezi kuwa na Mkurugenzi wa aina hiyo, haiwezekani Serikali iwekeze pesa kwa ajili ya kutoa maji kwa Wananchi halafu maji yapotee Wananchi hawana maji, Mkurugenzi wa aina hiyo tutakuweka pembeni na wala hatutokuwa na msalie Mtume”
“Wakati mwingine tunashangazwa kuona Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji anakwenda kumkatia mwananchi maji siku ya Sikukuu, unakwenda kumkatia Mwananchi maji Wikiendi haiwezekani, ni marufuku kumkatia Mwananchi maji siku ya Sikukuu au Wikiendi , tufuate taratibu na sheria, Mwananchi ana haki ya kutokatiwa maji Sikukuu au wakati wa mapumziko yake ya mwisho wa Wiki”