Leo February 27, 2020 Serikali mkoani Katavi imekamata silaha 50 zilizokuwa zinamilikiwa na baadhi ya Wakimbizi waliopewa uraia wa Tanzania kwenye makazi ya Mishamo na Katumba.
Silaha hizo zimekamatwa wakati wa operesheni inayojulikana kama safisha Katumba na Mishamo 2020 iliyofanyika kufuatia agizo lililotolewa na Rais John Magufuli kwa uongozi wa Mkoa huo wa Katavi.
Akitoa taarifa kuhusu operesheni hiyo Mkuu wa Brigedi ya Magharibi 202KV, Brigedia Jenerali Jacob Mkunda amesema kuwa silaha hizo zilikua zikimilikiwa na wakimbizi hao na kwamba zilikua zikitumiwa kufanya vitendo vya uhalifu.
Kufuatia kukamatwa kwa silaha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera na mkuu huyo wa Brigedi ya Magharibi 202KV wamewataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na vitendo vya uhalifu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kutokomeza vitendo hivyo.