Watu tisa wamefariki katika tukio la gari kusombwa na maji ya Mto Kisima eneo la Kijiji cha Lumeme Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma.
Akitoa taarifa leo March 12,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya amesema tukio hilo limetokea jana jioni baada ya gari hilo kusombwa na maji chanzo cha ajali kikiwa ni uzembe wa Dereva ambaye alilazimisha kuvuka wakati Mto huo ukiwa umejaa maji ambapo ametoa rai kwa Madereva na Wananchi kuacha tabia ya kupima maji katika madaraja kwa kutazama ili kuepuka ajali zisizotarajiwa.
RPC amesema “Gari lenye namba za usajili T.770 DBU aina ya Toyota Noah mali ya John Agathoni Kapinga wa Kijiji cha Lumecha likiendeshwa na Dereva Edwin Abel Ngowoko (55) likitokea Tingi kuelekea Nyoni lilisombwa na maji na kutumbukia Mtoni na kusababisha vifo vya Watu tisa ambao ni Edwini Abeli Ngowoko(55), Matengo (Dereva wa Gari), Valeliana Ndunguru (18), Innocent Cassian Ndunguru ( 63), Simon Mahai (21) na Nathan Kumburu (39)”
“Wengine waliofariki kwenye ajali hiyo ni Faraja Daud Tegete (18) ambaye ni Mwanafunzi wa kidato cha 3 Shule ya Sekondari Kilumba, Ebiati Daud Tegete ( 2) na Alfonsia Casian Mbele (40)”