Club ya Simba SC imemtambulisha mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana aliyekuwa anacheza Benchem United Augustine Okrah (28) kama mchezaji wao kwa mkataba wa miaka miwili.
Okrah ambaye amefanya vizuri msimu wa soka wa Ghana uliyomalizika kwa kufunga magoli 14 katika michezo 32 ya Ligi Kuu nchini Ghana, akimaliza nafasi ya tatu katika vinara wa mabao sawa na Bright Adjei wa Aduana Stars na Umar Bashiru wa Karela United 14, Okrah ni miongoni mwa wachezaji wawili wa Ligi ya ndani wanaoitwa Timu ya Taifa ya Ghana.
Augustine Okrah pia amefunga jumla ya magoli 3 katika mechi 5 za FA huku akiisaidia timu hiyo kufika hatua ya fainali FA, huku Ligi Kuu wakimaliza nafasi ya tatu ikiwa ni nafasi yao bora zaidi kuwahi kufika, kwa ujumla mashindano yote Okrah amecheza jumla ya mechi 37 na kufunga jumla ya magoli 17 sawa na wastani wa kukaribia kufunga goli moja kiła baada ya mechi.
Baada ya usajili huo wa Augustine Okrah sasa ni wazi kuna wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji wa kigeni wataachwa ndani ya kikosi cha Simba SC, hadi sasa Simba SC imetangaza kusajili jumla ya wachezaji watano, wakimataifa watatu Victor Akpan (Nigeria), Moses Phiri (Zambia) na Augustine Okrah (Ghana) na wazawa ni Nasorro Kapama na Habibu Kiyombo.