Baada ya tetesi za takribani mwezi mzima kuhusu usajili wa mfungaji bora wa ligi mfungaji bora wa Ligi ya Kenya Danny Sserunkuma, hatimaye klabu ya Simba imefanikiwa kumsajili mchezaji huyo na kuwazidi mbio wapinzani wao Yanga huku ikisitisha mkataba wa mchezaji wao mmoja wa kimataifa.
Kwa mujibu wa Makamu mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange, Jumatano ya wiki hii Simba itampa mkataba wa mwaka mmoja Sserunkuma na Mganda huyo atakuwa mchezaji halali wa klabu hiyo akichukua nafasi ya Kiongera ambaye uongozi wa timu hiyo umeona usitishe mkataba wake hadi apo atakapopona majeruhi yake anayokwenda kufanyiwa upasuaji India kesho.
“Tunasogeza mbele mkataba wa Kiongera hadi atakapopona majeruhi yake yatakayo tumia miezi mitatu baada ya upasuaji tutakua tunamfuatilia kwa karibu na nafasi yake ndiyo tumeona tumpe Sserunkuma ili kutimiza idadi ya nyota watano wa kigeni kama kanuni za TFF zinavyo tuagiza,”amesema Nyange.
Kiongera amejiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea KCB ya Kenya na ameichezea Simba mechi moja ya kwanza dhidi ya Coastal Union Septemba 21 akaumia baada ya kugongana kipa Shabani Kado dakika 89 na kutolewa nje.