Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameelezea kukoshwa na utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) inayolengwa kuzikwamua kaya masikini mkoani Iringa.
Ambapo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha zinafika kila mahali ikiwemo vijijini katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameyasema hayo wakati alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya Tasaf katika kijiji cha Kinywang’anga kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Tarafa ya Ismani ambapo amesema
” Nimeridhika na kufurahi sana na mradi huu wa Tasaf niliokuja kuutembelea,ni mradi ambao upo katika ofisi ya Rais, nikiwa kama msaidizi wake napita kukagua na kuona mmefanya vizuri acha niwapongeze,”
Kwa mujibu wa Simbachawene, miradi mingi ya Tasaf inasimamiwa vizuri na nia yake ni kuondoa umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kaya, ndio maana kunakuwa na wanufaika wa kupewa fedha za moja kwa moja ili kuwapa ahueni katika hali zao za maisha.
” Walengwa hawa hawafanyishwi kazi bali wanapewa fedha ili kujikimu, ” alisema.
Katika ziara hiyo alikagua mradi wa ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo uliopo Kinywanga’ nga akisifu na namna ulivyotekelezwa na kusema utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo wakiwemo wafugaji.
” Wafugaji wamenufaika lakini pia ustawi na huduma za kijamii katika eneo hili zinaendelea kukua,mifugo ikiwa mizuri hawa wanaohusika wanakuwa msaada mkubwa kwa jamii.Tasaf haigusi maisha ya masikini pekee bali maisha ya matajiri na wenye hali nzuri na mradi huu ni wa kipeee sana,”
“Kwa sababu ya hatua na msukumo utakaoletwa na Tasaf tunafikiri kwa siku za usoni tutaita mradi wa kuboresha maisha ya wananchi sio kuwasaidia masikini, nimeridhika na kufurahi sana kwa thamani ya Sh 4.8 milioni kwa mradi kama huu,” amesema Simbachawene.
Pia amesisitiza kuwa miradi inayotekelezwa na Tasaf inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na inawashikilisha wanajamii katika uhalisia wake akisema huo ndio msingi wa viongozi wa kitanzania.
Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda mfupi, Tasaf Ndugu Paul Kijazi amesema katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa kuna afua tatu katika jamii ikiwemo ya kuaulisha fedha inayowale wananchi wa kaya zisizokuwa na uwezo wa kufanya kazi wakiwemo wazee.
” Katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa tuna vijiji 134 vyote vinawaulishiwa fedha, tumeshaleta Sh 3.663 bilioni tangu katika awamu ya pili ya Tasaf kwa ajili ya walengwa.Lakini pia tulileta fedha kwa ajili ya vifaa Sh 1.09 bilioni vilivyotumika katika ajira za muda za mradi wa Tasaf.
Amesema utaratibu uliopo katika miradi ya ajira za muda, kuna fedha zinatangulia kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Pia alisema Tasaf imepeleka fedha kwa ajili ya watu waliofanya kazi kutoka katika kaya zilizoshiriki miradi.
” Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tumeleta Sh. 826milioni ni kama ujira kwa waliofanya kazi kwa muda mfupi kuanzia asubuhi hadi saa nne ili kushiriki shughuli zingine za uzalishaji mali.
” Pia tuna vikundi vya kuweka akiba ambapo katika halmashauri hii idadi ya kaya zilizojiunga ni 3600 na vikundi vilivyoanzishwa ni 265 na fedha zilizowekwa ni Sh 41 milioni zilizowekezwa kwenye vikundi,”
Hata hivyo amesema kuwa sababu ya kufanya hivyo ni mradi huo kuwa katika hatua mbalimbali ikiwemo uahulishaji kisha kupelekea maarifa na ujuzi kwa walengwa wanaoweza kufanya kazi, akisema ndio maana ya ajira za muda.
” Lakini vikundi hivi vinapata mafunzo na vimeshaweka akiba ya kujiendeleza, pia wanakuwa katika utaratibu wa kupewa mikopo inayowasaidia kujikwamua kiuchumi,” alisema Kijazi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu Mkoa wa Iringa, Mhe Halima Dendego, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Veronica Kessy amewataka wanufaika wa Tasaf kutunza miradi hiyo ili iwe endelevu kwa manufaa ya mifugo yao walioipata kupitia mpango huo.