Diego Simeone amekiri kuwa alikataa ofa ya Saudi Arabia ya kusalia Atletico Madrid.
Aliliambia gazeti la Marca: “Je, ofa ya Saudi ilinifanya kusita? Hapana, ukweli ni kwamba nina furaha sana pale nilipo. Nina furaha sana kuwa Atletico. Sikusita na ofa kutoka Saudi Arabia, si hata wakiongeza. Nina furaha Atletico.”
Kocha huyo wa Atlético Madrid, alipokea ofa nono ya kusimamia klabu ya Al Ahli ya Saudia, lakini vyanzo viliiambia ESPN kuwa hakuwa na mpango wa kuachana na kazi yake ya LaLiga.
Simeone alitia saini mkataba wa nyongeza miaka miwili iliyopita ambao utamfikisha mwisho wa msimu wa 2024 na amedokeza kuwa angependa kuendelea na klabu hiyo.
Simeone amekuwa meneja Atleti tangu 2011, na kumfanya kuwa mtu ambaye amefundisha timu kwa misimu mingi mfululizo kwenye La Liga.
Simeone, 53, aliifundisha River Plate miongoni mwa vilabu vingine vya asili yake Argentina na alikuwa na muda mfupi katika klabu ya Italia Catania kabla ya kuchukua mikoba ya Atlético.