Nchi ya Singapore imeiondoa Japan kwenye namba 1 ya orodha ya Nchi zinazomiliki passport zenye nguvu duniani baada ya Nchi hiyo kufikisha Nchi 193 ambazo Raia wake wanao uhuru wa kuingia bila kutakiwa kutuma maombi ya VISA kabla.
Wakati Singapore ikifikisha Nchi hizo 193 kati ya 227, nafasi ya pili nayo imechukuliwa na Ujerumani, Italia na Hispania ambazo zote kwa pamoja passport zao zimeongezewa nguvu kutokana na kufikisha Nchi 190.
Japan imeporomoshwa hadi nafasi ya tatu ambako imefungana na Korea Kusini, Austria, Finland, Ufaransa, Luxembourg na Uswizi ambapo Raia kutoka Nchi hizi 7 watafurahia uhuru wa kusafiri kwa kuingia Nchi 189 muda wowote wanaotaka bila kufata mlolongo mrefu ambao ingewalazimu kusubiri siku kadhaa kupata ruhusa ya VISA kabla ya kusafiri.
Mataifa maarufu duniani kama Marekani na Uingereza mara yao ya mwisho kushika nafasi ya juu kwenye chati hizi ilikua ni mwaka 2014 ambapo zote kwa pamoja zilifungana kwa kushika nafasi ya kwanza lakini kwa mwaka huu Marekani imeshika namba 8 ikiwezesha Raia wake kuingia Nchi 183 huku Uingereza ikishika namba 4.
Singapore ambayo hadi 2021 ilikua na Watu milioni 5.4 ilipata uhuru wake kutoka kwa Malaysia August 9 mwaka 1965.