Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema Zimbabwe haitamsahau aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli kwa kutenga Oktoba 25 kuwa siku ya kupaza sauti dhidi ya kuondolewa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.
Amesema wananchi wa Zimbabwe watamkumbuka Magufuli kwa msaada aliotoa kwa nchi hiyo baada ya kukumbwa na kimbunga Idai kilichoambatana na mvua kubwa.
Mnangagwa ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 22, 2021 katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa kuaga mwili wa kiongozi huyo atakayezikwa Ijumaa Machi 26, 2021 wilayani Chato Mkoa wa Geita.
“Sisi wananchi wa Zimbabwe tunamkumbuka sana kwa kuamua kutenga Oktoba 25 ni siku ya kupaza sauti dhidi ya vikwazo ambavyo Zimbabwe iliwekewa, historia yake itabakia alama katika eneo la Sadc pia haya aliyapitisha akiwa mwenyekiti wa Sadc.
“Mwaka 2019 tulikumbwa na kimbunga Idai, Zimbabwe na Malawi na alitoa tani nyingi za chakula. Nataka niwasimulie kilichotokea alinipigia simu usiku nikiwa nimelala nilipotambua ni Magufuli nilipokea simu hiyo aliniambia kaka yangu pole na kimbunga Tanzania inaweza kufanya nini ili kusaidia wananchi?”
“Nilimwambia ni chakula, mablanketi, dawa lakini baadaye nikasema unaweza kutusaidia vyandarua, siku ya pili jioni ndege ya Tanzania ilifika ikiwa na misaada hiyo,” Mnangagwa.