Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hataacha kusisitiza usitishwaji wa mapigano kwa sababu za kibinadamu huko katika Ukanda wa Gaza.
Antonio Guterre ameyasema hayo baada ya kushindwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio la kusitisha mapigano huko Gaza kutokana na kura ya veto ya Marekani.
Ibara ya 99 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambayo imetumika mara 9 pekee katika historia ya umoja huo, inamruhusu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo kubwa zaidi duniani kuwaita wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye mkutano wa dharura wakati anapohisi kwamba “amani na usalama wa dunia” uko hatarini na kuwataka wachukue hatua za haraka kuhusu suala hilo.
Antonio Guterres akizungumza katika mkutano wa Doha, mji mkuu wa Qatar, Guterres amekiri kwamba “vita vya Gaza vimedhoofisha uaminifu na uhalali wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”
Muswada wa kusitishwa mashambulizi ya Israel dhidii ya watu wa Ukanda wa Gaza ulipigiwa kura usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama uliofanyika New York, na kupasishwa na wanachama 13 kati ya 15 wa baraza hilo. Marekani imeupinga kwa kura ya veto huku Uingereza ikijizuia kupiga kura.
Muswada huo ulitoa wito wa “kusitishwa mapigano mara moja kwa sababu za kibinadamu” na kuungwa mkono na nchi za Kiarabu na Kiislamu.