Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Joseph Kilangi ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupeleka umeme wa uhakika katika Kisiwa cha Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa 06 Desemba, 2023 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Tanzania Bara pamoja na Wizara ya Maji, Nishati na Madini kutoka Zanzibar.
Amesema kuwa Zanzibar kuna umeme wa uhakika kutoka TANESCO ambalo ni Shirika lililopo chini ya Wizara ya Nishati, hali ambayo imeendelea kuimarisha Sekta ya Utalii Zanzibar pamoja na shughuli nyingine za maendeleo.
“Kwa matumizi bora ya umeme nawashauri watanzania wote kutoka Zanzibar na Tanzania bara kuwa na matumizi bora ya umeme kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme mdogo, kuliko kutumia vifaa ambavyo vinatumia umeme mwingi bila sababu,” amesema Kilangi.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, CPA. Michael Marandu amesema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa ni MW 1,872.05 na kiasi hicho kinatokana na vyanzo mbalimbali.