Somalia imepokea dozi milioni 1.4 za chanjo ya matone ya kipindupindu zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2.5 kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), wakati wasiwasi ukiendelea kutokana na kuongezeka kwa idadi ya kesi za ugonjwa huo zinazoripotiwa nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na UNICEF mjini Mogadishu jumamosi jioni imesema, chanjo hizo zitasambazwa katika wilaya tano zenye maambukizi zaidi nchini humo, ikiwa ni katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo ambao tangu mwezi Januari umewapata watu 4,388 na kusababisha vifo vya watu 54, wengi wakiwa watoto.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya kesi zilizoripotiwa mwaka huu nchini Somalia ni za juu kwa mara tatu zaidi ya kesi zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho katika miaka mitatu iliyopita.
Ongezeko la maambukizi ya kipindupindu linatokana kwa kiasi kikubwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El Nino mwishoni mwa mwaka jana, ambazo zilisababisha vifo vya watu 118 na wengine milioni 1.2 kukosa makazi.