Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akiambatana na timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amefanya ziara ya kikazi kwenye ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tarehe 20 Februari, 2019.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukutana na Maafisa wa Taasisi za Serikali wanaohudumia wawekezaji kupitia Mfumo wa Mahala Pamoja. Alitumia ziara hiyo kusikiliza namna ambavyo Maafisa wanavyofanya kazi zao ndani ya Mfumo ili kujifunza na baadae kutoa maagizo ya kuboresha utoaji wa huduma husika kwa Wawekezaji.
Ziara hiyo imekuja zikiwa zimepita takribani siku tano tu baada ya Waziri kukutana na Watumishi wa TIC na kufanya nao mkutano kwa kila idara kwa lengo la kujifunza majukumu ya kila idara, kufahamu changamoto, kupokea mapendekezo ya kuboresha utekelezaji wa majukumu hayo na kutoa maelekezo ya kuchapa kazi kwa kufuata misingi ya weledi.
Baada ya Waziri kukaribishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe kwenye ofisi za Huduma za Mahala Pamoja, alikaa kwa muda wa masaa manne na amekutana na mfanyakazi mmoja mmoja anayewakilisha Taasisi zinazofanya kazi ndani ya Mfumo wa Mahala Pamoja ambapo alipokea taarifa ya majukumu na ripoti ya utekelezaji.
Katika ziara hiyo, Waziri amekuta TIC inatekeleza mfumo wa kielektroniki (TIW) ambao unatumiwa kupokea na kuchakata maombi ya wateja kwa ajili ya cheti cha uwekezaji. Waziri alivutiwa na taarifa ya kutumika kwa mfumo na akahitaji kufahamu iwapo mfumo unatumika kwenye ofisi zote za TIC zikiwemo zile za Kanda.
Maelezo yalitolewa kwamba kwa sasa mfumo huo unatumiwa TIC Makao Makuu na kwenye Kanda moja ya Kaskazini na zoezi lipo mbioni kukamilika kwenye kanda zilizobaki.
Kufuatia maelezo hayo, Kairuki ameagiza TIC ikamilishe ndani ya mwezi mmoja kuunganisha mfumo huo katika Kanda ambazo bado ili pia ziweze kuchakata maombi ya wawekezaji kielektroniki.
“Ni wazi mfumo huo unasaidia kuondokana na urasimu, ucheleweshwaji na unarahisisha upatikanaji wa huduma nyingine ambazo ni upatikanaji wa leseni, cheti na vibali ambavyo mwekezaji anahitaji ili kuanzisha mradi wa uwekezaji nchini’ Kairuki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Geoffrey Mwambe alisema iwapo Serikali itawezesha taasisi zote zinazohusika na huduma za mahala pamoja kutoa idhini huduma mbalimbali za uwekezaji ndani ya ofisi za TIC itakuwa ni hatua kubwa uwekezaji nchini.
“Taasisi zilizopo ndani ya mfumo wa mahala pamoja zinafanya kazi kubwa, tunachoomba sisi kama TIC ni kwamba huduma za taasisi hizo kwa wawekezaji zikamilike ndani ya TIC badala ya kwenda kwenye makao makuu ya ofisi hizo kufuata idhini ya vibali, leseni na vyeti husika kwa wawekezaji” Mwambe.
Katika mazungumzo yake na wawakilishi wa idara, Waziri aliwataka watendaji wa ardhi ndani ya Kituo hicho kuweka vizuri takwimu za ardhi ya uwekezaji na kushughulikia changamoto za upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji .
Akiwa katika sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Waziri Kairuki aliagiza watendaji hao kuona umuhimu wa utoaji wa cheti cha walipakodi wakubwa (VAT) ndani ya Kituo ili kurahisisha huduma kwa wawekezaji.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa wawekezaji Anna Lyimo amesema kwa sasa huduma za mahala pamoja zimekuwa na manufaa makubwa kwa wawekezaji kutokana na kuwapo kwa taasisi nyingi muhimu Kituoni ambazo zinamuwezesha kupata huduma husika na kwamba marekebisho yaliyotajwa na Waziri yatafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.
“Tumeyapokea maagizo ya Waziri na tutayafanyia kazi, ni maagizo yenye tija kwa kituo” Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Mahala Pamaoja wa TIC Anna Lyimo.
KUTOKA IKULU: TANZANIA KUPEWA KIFUTA JASHO CHA BILIONI 682.5