Simba saba wamekutwa wameuawa katika Hifadhi ya Jamii ya Ikona (WMA) wilayani Serengeti, mara baada ya mfugaji mmoja wa Park Nyigoti kudaiwa kuwatega kwa sumu kufuatia ng’ombe wake mmoja kukamatwa malishoni ndani ya hifadhi hiyo.
Askari wa pori la akiba wakiongozana na mfugaji mmoja walibaini mizoga ya simba hao katika eneo ambalo inasemekana alikamatwa ng’ombe wa mfugaji huyo.
Mtuhumiwa wa tukio anasakwa baada ya kukimbia, ambapo thamani ya simba hao imetajwa kuwa ni jumla ya shilingi milioni 175.
Daktari aliyewafanyia uchunguzi simba hao amebaini kuwa sumu waliyopewa ilisababisha damu kuvujia ndani, na kwa sasa wanasubiri vipimo kutoka kwa mkemia mkuu.
MWANANCHI
Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu amesema anaamini rais ajaye ni kijana, na kuongeza kuwa sio kosa iwapo Rais Kikwete atakabidhi kijiti kwa mtu mwenye umri kama wake.
Nyalandu amesema wakati haujafika kwa yeye kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia CCM kama ambavyo imekuwa ikisemekana.
Wakati huohuo amepinga shutuma ambazo zinazushwa juu yake kuwa ameuza baadhi ya hifadhi za taifa, na kusema shutuma hizo zinatokana na msimamo wake katika vita dhidi ya ujangili.
Amesema jimbo lake kwa sasa ndio linaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula mkoa wa Singida ikiwamo vitunguu vinavyouzwa ndani na nje ya nchi.
MTANZANIA
Serikali imetoa onyo kwa wasimamizi wa mitihani watakaowasaidia watahiniwa kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne, na kwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Jenista Mhagama ambapo tarehe 3 Novemba wanafunzi takribani 297,488 wanatarajiwa kuanza mitihani ya kumaliza kidato cha nne Tanzania.
Idadi hiyo ya watahiniwa inatajwa kuwa ni pungufu kwa asilimia 13.3% ikilinganishwa na wanafunzi waliofanya mitihani hiyo mwaka 2013.
Naibu Waziri huyo amesema kutokana na maoni ya wadau mbalimbali mfumo wa mitihani ya watahiniwa wa kujitegemea kuanzia mwaka huu watakuwa wakifanya mitihani karatasi mbili kwa kila somo, utaratibu ambao wahusika walishapewa taarifa mapema kuhusiana na utaratibu huo.
NIPASHE
Kumekuwepo na uvumi kwamba taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imekuwa ikiwakata majeruhi wa ajali za bodaboda hasa madereva kama njia ya kuwakomesha ambapo taasisi hiyo imekanusha vikali juu ya hilo.
Afisa habari wa MOI Patrick Mvungi amepinga uvumi huo na kusema kila mgonjwa anayefika katika taasisi hiyo hutibiwa kulingana na vipimo na ushauri wa madaktari.
Taasisi hiyo ina wastani wa kupokea majeruhi 600 kila mwezi na kati yao zaidi ya 300 ni wale waliotokana na ajali za bodaboda, daktari mmoja ambaye ametaka jina lake lisitajwe amesema kwa majeruhi yoyote aliyevunjika hakuna namna ya mgonjwa huyo kuikwepa MOI kwa kuwa hakuna hospitali inayotoa huduma ya uunganishwaji wa mishipa na mifupa zaidi ya MOI kwa Tanzania.
Mmoja ya wagonjwa waliolazwa katika taasisi hiyo ambaye alipata ajali ya bodaboda amesema alikubaliana na madaktari kumkata mguu huo kutokana na kushindikana kuungika na kusema kuwa hakukatwa kwa kulazimishwa.
NIPASHE
Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya mji Masasi, Mtwara kilishindwa kuendelea baada ya kuvunjika ghafla kutokana na madiwani hao kugomea kuthibitisha ajenda kwa kile kilichodaiwa kuwa Mkurugenzi wa halmashauri pamoja na menejimenti wameshindwa kutekeleza maazimio mbali mbali.
Madiwani hao walisema baadhi ya maazimio hayajatekelezwa na yalipaswa kufanyiwa kazi kabla ya kufanyika kwa kikao hicho.
Aidha wamesema sababu nyingine ni pamoja na kutokuridhishwa na taarifa za mchanganuo wa matumizi ya ALAT ambapo walidai zipo kasoro nyingi zilizojitokeza kwenye makablasha waliyopewa kujadili.
JAMBO LEO
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa wiki mbili kwa maofisa wa Mamlaka ya Bandari (TPA) kutoa taarifa kuhusiana na namna walivyotumia sh. Bilioni 9.6 kufanya kikao kimoja cha wafanyakazi wake.
Makamu mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe amesema baada ya CAG kumaliza kukagua hesabu za mamlaka hiyo alikabidhi ripoti yake kwa kamati hiyo kwa hatua zaidi ambapo kulikuwa na mambo ambayo TPA ilipaswa kutolea maelezo ikiwemo matumizi ya sh. bilioni 9.6 kwa ajili ya mkutano, sh. bilioni 6.4 kwa ajili ya matangazo na bil. 10 kwa ajili ya safari.
Mwenyekikti wa bodi ya TPA, Profesa Joseph Msambichaka amesema ripoti ya CAG kuhusiana na uchunguzi wa fedha hizo waliipata juzi, hivyo ameiomba kamati hiyo muda wa kusoma kabla ya kujieleza mbele ya kamati ya PAC.
UHURU
Mtangazaji wa zamani wa iliyokuwa Redio Tanzania (RTD) kwa sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ben Kikoromo maarufu kama ‘Ben Kiko’ amefariki dunia usiku wa Novemba 30 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa magonjwa mbali mbali ikiwemo figo.
Mtoto wa marehemu, Said Kikoromo amesema baba yake alikuwa akisumbuliwa na homa pamoja na tatizo la miguu na baadaye akaanza kuumwa figo, na kuhamishwa kutoka hospitali ya Hospitali ya Mirambo, Tabora kwenda Muhimbili ambako mauti yalimkuta akiwa anapata matibabu.
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, Kuomboleza kifo cha Ben Kiko na kusema kifo hicho kiwe chachu ya wanataaluma husika kujituma zaidi na wawe tayari kuiga mazuri aliyoyafanya enzi za uhai wake.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook