Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kikosi cha kupambana na wizi wa mifugo (STPU) na Bodi ya nyama Kanda ya Kaskazini leo wamefanya ukaguzi wa hali za maduka yanayouza nyama (BUTCHER) katika sokuu jijini Arusha.
Akiongea na wauzaji wa maduka hayo na wateja Kamanda wa Polisi Kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini Kamishna msadizi wa Polisi ACP Simon Pasua amesema kuwa wapo katika ukaguzi wa kawaida ambao wamekuwa wakiufanya mara kwa mara katika maduka hayo lengo likiwa ni kubaini mapungufu na kutoa maelekezo ili kuweka mazingira bora ya walaji.
ACP Pasua amebainisha kuwa yapo mapungufu ambayo wahusika wa maduka wanapaswa kuyafanyia kazi kwa wakati ili kutoleta changamoto kwa binadamu huku akiwataka kupeleka mifugo katika machinjio yanayotambulika na bodi ya nyama kanda ya kaskazini.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa bodi ya nyama kanda ya kasikazini Patrick Kaaya amesema kuwa wao kama bodi ya nyama wanafahamu bidhaa hiyo ilivyo muhimu kwa Maisha ya binadamu ambapo amesisitiza kwa wauzaji wa maduka hayo kuwa makini na bidhaa hiyo ambayo ni nzuri kwa ajili ya kulinda afya ya walaji huku akiwataka wale wenye nia mbaya na biashara hiyo kuacha mara moja.
Nae Mfanyabiashara wa duka la nyama bwana Wilfred Moleli amesema kuwa wao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa uaminifu mkubwa huku akibanisha kuwa wao wanafanya biashara hiyo kwa mujibu wa sheria bila kuvunja taratibu za bodi ya nyama.
Kiongozi wa soko kuu la Jiji la Arusha Francis Haule amesema bodi hiyo na kikosi kina pasaswa kuendelea kutoa elimu licha ya kupongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya kikosi cha STPU na Bodi hiyo amewataka wafanyabiashara wa soko hilo ikiwemo wa maduka ya nyama kufuata taratibu za bodi hiyo.