Serikali imesema kuwa katika kutambua wanawake wanaobebeshwa mimba na kuachwa bila matunzo, imeandaa sheria ya mtoto inayotoa maelekezo kwa wazazi kuhakikisha kuwa mtoto anapata matunzo yote stahiki ili kuhakikisha kuwa haki na ustawi wake vinatimizwa.
Hayo yamebainishwa Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Mwanaidi Hamis, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Neema Lugangira, aliyehoji ni upi mkakati wa serikali katika kuwakomboa wanawake wanaogharamia malezi ya watoto peke yao bila Baba kuwajibika.
“Serikali imetoa maelekezo wazazi kuhakikisha mtoto anapata matunzo yote stahiki, na kama wazazi wa mtoto hawaishi pamoja na mtoto anaishi na Mama yake basi Baba atawajibika kugharamia malezi ya mtoto kulingana na kipato alichonacho, sheria hii pia imesaidia kuhakikisha suala la gharama kwa mtoto linawagusa wazazi wa pande zote mbili”, Naibu Waziri wa Afya Mwanaidi Hamis