Mapigano yameendelea katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa Sudan Khartoum kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa RSF wakati huu mzozo baina ya pande hizo ukiwa unaendelea.
Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye ukurasa wa facebook siku ya Jumanne, jeshi lithibitisha kuzuia shambulio lengine na wapiganaji wa RSF kwenye kambi yake katika eneo la Al-Shajara, kusini mwa Khartoum.
Aidha jeshi la serikali lilisema limetekeleza uharibifu mkubwa kwa kundi la RSF.
Kwa upande wake wapiganaji wa RSF kupitia ukurasa wa X zamani ukijulikana kama twitter, walidai kuchukua udhibiti wa baadhi ya maeneo katika kambi hiyo pamoja na kuchukua silaha za kijeshi.
Televisheni ya AI Arabiya inayofadhiliwa na serikali ya Saudi katika mtandao wake iliripoti kuwa jeshi lingali linadhibiti kambi hiyo baada ya siku tatu za mapigano makali.
Mapigano kati ya vikosi viwili nchini humo yameongezeka katika muda wa hivi karibuni katika mji mkuu wa Khartoum na miji jirani ya Omdurman na Bahri sawa na sehemu zengine zinazokabiliwa na machafuko Magharibi mwa mji wa Darfur.