Mapigano makali kati ya Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF yameendelea kushuhudiwa jijini Khartoum, wakati huu kukiwa na wasiwasi wa kuzuka kwa magonjwa kama utapiamlo miongoni mwa watu waliokimbia makaazi yao huku vita katika mji mkuu wa nchi hiyo na maeneo ya magharibi vikiingia wiki ya 12, bila dalili zozote za kumalizika kwa mzozo huo kwa amani.
Makabiliano yalianza kushuhudiwa Jumapili asubuhi Kaskazini mwa jiji la Khartoum, baada ya wanamgambo wa RSF kujaribu kushambulia maeneo yanayodhibitiwa na wanajesjhi wa Sudan.
Milio ya risasi na mashambulio ya angaa yalishuhudiwa pia Mashariki mwa jiji hilo kuu, huku wanamgambo wa RSF wakidai kuangusha ndege ya jeshi katika eneo la Bahri, Kaskazini mwa Khartoum.
RSF ilisema iliangusha ndege ya kivita ya jeshi, na ndege isiyo na rubani huko Bahri, katika taarifa ambazo jeshi halikudhibitisha mara moja.
“Tunaogopa, kila siku mashambulisi yanazidi kuwa mabaya,” Nahid Salah mwenye umri wa miaka 25, anayeishi kaskazini mwa Omdurman, alisema katika mahojiano ya simu na shirika la habari la Reuters.
RSF imedhibiti, kwa kiasi kikubwa, ardhi ya mji mkuu, na imeshutumiwa kwa uporaji na kuchukua nyumba kwa lazima, wakati jeshi likilenga zaidi, kufanya mashambulio ya anga na kutumia mizinga.